Leo tarehe 17 Januari 2022, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewasilisha rasmi kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika Hati ya kuridhia Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (CFTA). Hati hiyo imewasilishwa na Mhe. Innocent Eugene Shiyo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Afrika.
Hatua hii imekuja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Azimio Na.4/2021 la tarehe 09 Septemba 2021 linalotoa idhini ya Tanzania kuwa sehemu ya Mkataba wa Soko la Pamoja la Bara la Afrika.
Balozi Shiyo amewasilisha hati hiyo kwa Mhe. Balozi Albert Muchanga, Kamishna wa masuala ya Uchumi, Biashara, Viwanda na Madini wa Umoja wa Afrika ambaye ameipokea kwa niaba ya Mhe. Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika.
Wakati wa kuwasilisha Hati hiyo Mheshimiwa Balozi Shiyo alisisitiza kuwa kuanzishwa kwa Soko la Pamoja la Afrika ni fursa na hatua muhimu sana katika kupanua fursa za biashara, kuvutia wawekezaji na kuongeza mauzo ya bishaa za Tanzania hasa bidhaa za kilimo. Aliendelea kufafanua kuwa fursa hizi zitakuwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi na biashara baina ya nchi wanachama (intra-African trade) kwa kukuza ushiriki wa Afrika katika biashara ya dunia na kujenga uwezo wa kuongeza thamani ya bidhaa kupitia sera bora za kukuza teknolojia, ubunifu na ushindani.
Balozi Shiyo alisisitiza utayari wa Tanzania kushiriki kikamilifu kwenye utekelezaji wa Mktaba wa AfCFTA ambao unafungua milango ya soko la pamoja la zaidi ya watu Bilioni 1.3 barani Afrika.
Kwa upande wake, Kamishna Balozi Muchanga ameipongeza Tanzania kwa kuridhia na kuwasilisha kwenye Kamisheni ya Umoja wa Afrika Hati ya kuridhia Mkataba wa AfCTA na kutoa wito kwa nchi nyingine ambazo bado hazijaridhia mkataba huo kufuata mfano wa Tanzania.
Mkataba huu umesainiwa na jumla ya nchi wanachama wa umoja wa Afrika 54 kati ya 55 na ulipata hadhi ya kisheria Julai 2019 baada ya kuridhiwa nan chi Wanachama 28 wa Umoja wa Afrika.
