Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabiti Kombo, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mkutano wa 1303 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, uliofanyika kwa ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali, tarehe 24 Septemba, 2025 jijini New York, Marekani.
Mkutano huo, ambao umefanyika pembezoni mwa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 80), umebeba kaulimbiu isemayo: 'Kuchochea Upya Juhudi za Kuzuia na Kutatua Migogoro Barani Afrika.
Akizungumza katika mkutano huo, Mhe. Waziri Kombo amesema kuwa kaulimbiu hiyo imekuja wakati muafaka, ambapo Tanzania inaendelea kutekeleza azma yake ya kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kulinda amani na kutatua migogoro kwa kuzingatia misingi ya diplomasia.
Ameongeza kuwa Viongozi wengi Barani Afrika wanatambua mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha miundombinu ya amani na usalama kupitia utekelezaji wa Miundombinu ya Amani na Usalama ya Afrika, pamoja na Miundombinu ya Utawala Bora.
“Hatua hii imewezesha kuanzishwa kwa majukwaa ya kubadilishana maarifa kati ya Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika, na hivyo kuimarisha mshikamano pamoja na dhamira ya pamoja ya kuiwezesha Afrika kufikia amani ya kudumu katika siku zijazo,” alifafanua Mhe. Waziri Kombo.
Amesema kuidhinishwa kwa Azimio la Solemn mnamo Mei 2013, wakati wa maadhimisho ya Miaka 50 ya Umoja wa Afrika, bara la Afrika liliweka lengo la kumaliza vita ifikapo mwaka 2020 kupitia mpango wa Kukomesha Silaha (Silencing Guns).
Kutokamilika kwa azimio hilo kulisababisha kuongeza muda wa utekelezaji wa azimio hilo hadi mwaka 2030, ili kuwezesha Afrika kufikia dhamira ya pamoja ya kuleta amani ya kudumu Barani Afrika.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika, Rais João Lourenço wa Angola, amewataka nchi wanachama kuimarisha juhudi za kuzuia na kutatua migogoro barani Afrika ili kuimarisha usalama wa Waafrika na maendeleo.
“Ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa sasa, migogoro hii itaendelea kuhatarisha amani na utulivu wa bara, na pia kuzuia utekelezaji maazimio na mikataba ya Umoja wa Afrika chini ya Ajenda 2063 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa,” alisisitiza Rais Lourenço.
Ajenda 2063 ni mpango wa muda mrefu wa maendeleo wa Umoja wa Afrika (AU) uliobuniwa mwaka 2013 wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa AU, ili kuimarisha ustawi, amani, umoja, na maendeleo jumuishi ya Bara la Afrika ifikapo mwaka 2063.
Rais Lourenço pia alisisitiza umuhimu wa kuongeza michango ya kifedha katika Mfuko wa Amani wa Umoja wa Afrika uliohuishwa, na kushirikiana na Umoja wa Mataifa katika kutekeleza Azimio la Baraza la Usalama la UN namba 2719, ili kuweka misingi imara ya rasilimali zitakazosaidia jitihada za kuleta amani barani Afrika.
Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika lilianzishwa mwaka 2004 kama sehemu ya taasisi za Umoja wa Afrika iliyolenga kudumisha amani, usalama, na utulivu barani Afrika.
Baraza hili pia linawajibika kuzuia migogoro kabla haijatokea, kushughulikia migogoro inayojitokeza, na kutafuta suluhisho la kudumu kwa migogoro iliyopo ili kuleta maendeleo endelevu na ustawi wa Bara la Afrika.
Mkutano huu ulihudhuriwa na nchi zote Wanachama wa Baraza la Amani na Usalama, Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.















