Mheshimiwa Innocent Eugene Shiyo, Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA) amewasilisha Hati za Utambulisho leo tarehe 5 Januari, 2022 kwa Mheshimiwa Sahle- Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia.
Katika mazungumzo yao, Mheshimiwa Rais Zewde alimkaribisha Balozi Shiyo nchini Ethiopia na kumpongeza kwa kuteuliwa kuiwakilisha Tanzania nchini Ethiopia. Aidha, alisifia mahusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Ethiopia uliojengwa na waasisi wa mataifa haya mawili, Hayati Baba wa Taifa, Julius Kambarage Nyerere na Mfalme Haile Selassie, ambao walifanya kazi pamoja kuanzisha Umoja wa Afrika
Aidha, Mheshimiwa Rais Zewde aliishukuru Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono Ethiopia kwenye masuala mbalimbali ya kikanda na kimataifa ikiwemo kwenye suala la matumizi ya maji ya Mto Nile chini ya ushirikiano wa Nchi za Bonde la Mto Nile.
Vilevile, Mheshimiwa Rais Zewde aliipongeza Tanzania kwa kuendelea kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Ethiopia za kuhakikisha changamoto za usalama nchini Ethiopia zinapata ufumbuzi. Pia, alimuahidi Mhe. Balozi Shiyo ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu yake wakati wote atakapokuwepo nchini Ethiopia.
Kwa upande wake, Mhe. Balozi Shiyo aliishukuru Serikali ya Ethiopia kwa mapokezi na ukarimu alioupata tangu kuwasili kwake nchini Ethiopia tarehe 26 Novemba, 2021. Aidha, aliwasilisha Salamu za heri kutoka kwa Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenda kwa Mheshimiwa Sahle- Work Zewde, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Ethiopia.
Aidha, Mhe Balozi Shiyo alirejea mafanikio ya ziara ya Mhe. Rais Sahle-Work Zewde alioifanya nchini Tanzania mwezi Januari 2021 ambapo nchi zetu mbili zilikubaliana kuimarisha ushirikiano kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo biashara na uwekezaji, uchukuzi, nishati, mifugo na bidhaa za Ngozi, utalii, uhamiaji na ulinzi na usalama. Mhe. Balozi Shiyo aliahidi kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kuimarsha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili kwenye maeneo hayo na maeneo mengineyo yenye manufaa kwa pande zote mbili. Vilevile aliongelea kuhusu suala la kuanza kufundisha lugha ya Kiswahili kwenye Chuo Kikuu cha Addis Ababa kupitia ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Addis Ababa.
Mwisho, Mhe. Balozi Shiyo alimhakikishia Mheshimiwa Rais Zewde kwamba Tanzania itaendelea kuunga mkono Ethiopia kwenye jithada za kurejesha amani na usalama nchini humo.




