Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete ametunukiwa tuzo ya kiongozi bora wa mwaka 2023 katika Tuzo za Kiongozi Bora wa Afrika kwa Mwaka 2023 (African Leadership Person of the Year) kama Kiongozi Bora wa Mwaka katika Amani na Usalama barani Afrika.
Katika hotuba yake Mh. Kikwete wakati wa hafla hiyo iliyoandaliwa na Jarida la Uongozi Afrika (ALM), na kufanyika Addis Ababa usiku wa Machi 15, 2024, Dkt. Kikwete ameshukuru kwa kutunukiwa tuzo hiyo na kuwasihi Waafrika wote kwenye nafasi za uongozi kutoa kipaumbele kwenye masuala kutatua changamoto zilizopo ikiwemo umasikini, changamoto ya chakula, mabadiliko ya tabia ya nchi, magonjwa, ujinga, migogoro ya kisiasa na vita.
“Ukweli ni kwamba, ni kwa heshima kubwa ninakubali kupokea tuzo hii. Naipokea,
si tu kwa ajili yangu bali kwa niaba ya Waafrika wengine wengu – wawe viongozi wa kisiasa, wenye ushawishi kiuchumi, viongozi wa dini, wanachama wa vikosi vya usalama, watumishi wa umma, na wananchi wa kawaida - ambao huamka kila siku na kufanya sehemu yao katika kulifanya Bara la Afrika kuwa sehemu nzuri zaidi
ya kuishi,” amesema Dkt. Kikwete.
Rais Kikwete pia amepongeza juhudi zinazofanywa na Afrika katika kupiga hatua kimaendeleo hususa mapinduzi makubwa katika kuboresha elimu.
Kutunukiwa tuzo hii ni kufuatia mchakato uliojumuisha mapendekezo ya majina pamoja na kura zilizopigwa mtandaoni kwa wale waliopendekezwa, huku Kikwete akiibuka na ushindi wa asilimia 60.
Pamoja naye, Mtanzania Jesca Nkwabi pia amepokea tuzo ,ya uongozi bora.