Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimesaini makubaliano maalum (Memorandum of Understanding on Academic and Research Cooperation between the University of Dar es Salaam and the the University of Addis Ababa). Makubaliano hayo yamesainiwa tarehe 9 Februari, 2022 katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa. Makubaliano hayo yalisainiwa na Prof. William A.L. Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Prof. Tassew Woldehanna, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa.  Mchakato wa kuanza kufundisha Kiswahili katika Chuo kikuu cha Addis Ababa ni wa muda mrefu lakini ulianza kupata msukumo wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn tarehe 31 Machi, 2017 ambapo Viongozi Wakuu wan chi hizi mbili waliweza kubadilishana mawazo namna ya kuenzi Kiswahili kama moja ya lugha inayozungumzwa zaidi Barani Afrika. Mchakato huu ulipata nguvu zaidi wakati wa ziara ya Kiserikali  ya Mh.  Sahle - Work Zewde Rais wa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Shirikisho la Watu wa Ethiopia aliyoifanya nchini Tanzania Januari 25,2020. Wakati wa Ziara hiyo Viongozi wetu walikubaliana kimsingi Kiswahili kianze kufundishwa katika Chuo Kikuu cha Addis Ababa kwani pamoja na kuwa ni lugha ya Taifa Tanzania, bado kimekuwa ni kiunganishi kikubwa kwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki, ambapo kimekuwa kiungo muhimu cha shughuli mbalimbali ikiwemo biashara na utamaduni duniani.  Wakati wa ziara hiyo Mh. Rais Zewde alisema kuwa juhudi hizi ni muendelezo wa juhudi zilizokuwepo za kuifanya lugha ya Kiswahili kama lugha ya bara la Afrika. “Tulikuwa na mchakato wa kutaka Kiswahili kiwe lugha inayotumika Afrika. Nashukuru sana na tutakuwa tayari kuwapokea walimu kutoka Tanzania kwa ajili ya kufundisha Kiswahili Ethiopia,” Alisema Mhe. Rais Zewde

Lugha ya Kiswahili imekuwa na historia ya muda mrefu kwa Tanzania na Afrika. Kama Taifa, kumekuwa na michakato mbalimbali ya kukikuza na kukieneza Kiswahili Duniani. Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa Kiswahili ni lugha ya kujenga umoja na mustakabali wa maendeleo ya Afrika. Ni katika harakati hizo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeona haja ya kutumia lugha ya Kiswahili kama mojawapo ya lugha ya kazi za Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika uliofanyika tarehe 5-6 Februari 2022 nchini Ethiopia, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isidor Mpango alihutubia kwa lugha ya Kiswahili na kutoa ombi la lugha hiyo kuwa lugha ya kazi ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Aidha alitoa kiasi cha dola za Kimarekani laki mbili na nusu (250,000) ikiwa sehemu ya nia na utayari wa Tanzania katika azma hiyo. 

Kama sehemu ya utekelezaji wa kufanikisha Kiswahili kuwa lugha ya kazi ya Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia ulialika taasisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).  Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimejiandaa kikamilifu kwa rasilimali watu na fedha kwa ajili ya kufundisha, kutafiti, kuchapisha na kutoa wataalamu wa Kiswahili kwa watumishi wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Ethiopia na nchi za Afrika kwa ujumla. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia kimeanzisha programu za kufundisha Kiswahili kwa wanafunzi kutoka nchi za Afrika kwa kutoza ada sawa na Watanzania ambayo ni takribani dola za Kimarekani mia nne tu kwa mwaka. Vilevile kimeanzisha ufadhili wa masomo kwa wanafunzi kutoka nchi za Afrika ambapo Kiswahili hakitumiki sana kusoma shahada ya Umahiri ya Kiswahili bure katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Kwa upande wa Baraza la Kiswahili la Taifa, limejiandaa kikamilifu kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na taasisi nyingine husiani kuwa mstari wa mbele kama chombo cha ithibati ya Kiswahili cha taifa kuhakikisha Taifa linafikia azma lengwa. 

Ni kwa muktadha huo ujumbe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ukiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo Prof. William A. L. Anangisye pamoja na ujumbe wa BAKITA ukiongozwa na Katibu Mtendaji Bi. Consolata Mushi umefanya ziara rasmi jijini Addis Ababa, Ethiopia na kupokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia Mheshimiwa Balozi Innocent Shio na kufanya mazungumzo ya pamoja hasa kuhusu mikakati na utayari wa kazi iliyo mbele yetu. Pamoja na mambo mengine ya kimkakati ujumbe wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam utakutana na Uongozi wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa na uongozi wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika. Mikakati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ni pamoja na kusaini Hati ya Mkataba wa Mashirikiano na Chuo Kikuu cha Addis Ababa pamoja na vyuo vingine katika bara la Afrika. Aidha, Chuo kilikutana na Jumuiya ya Kiswahili nchini Ethiopia na kufanya mazungumzo ya pamoja ya kimkakati ya kuratibu ufundishaji wa Kiswahili katika jamii za Ethiopia. Ubalozi unafanya kila juhudi kuhakikisha mipango ya taasisi zote mbili na serikali kwa ujumla inafanikiwa kwa kiwango cha juu.

Prof. William A.L. Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa niaba ya Uongozi wa Chuo na Watumishi wote kwa ujumla aanatoa shukrani za kipekee kwa Balozi Innocent Shiyo kwa juhudi zake binafsi alizochukua kwa kipindi kifupi tangu ateuliwe kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Afrika na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi BArani Afrika kwa kufufua juhudi za kutialiana saini mktaba huo na zaidi kwa kuhakikisha kuwa Kiswahili kinakuwa ni moja ya ajenda katika Mkutano wa 35 wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliyomalizika hapa Addis Ababa tarehe 6 Febbruari, 2022. 

  • Prof. William A.L. Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (kushoto) na Prof. Tassew Woldehanna, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa wakibadilishana nakala za makubaliano yaliyosainiwa
  • Prof. William A.L. Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Prof. Tassew Woldehanna, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa wakisaini makubaliano ya ushirikiano
  • Prof. William A.L. Anangisye, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Prof. Tassew Woldehanna, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa wakizungumza na vyombo vya habari baada ya kusaini makubaliano ya ushirikiano